‘Yanga inapindua meza’

‘Yanga inapindua meza’

By Eliya Solomon

LICHA ya Yanga kukumbana na kipigo cha bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United, inawezekana kwa vijana hao wa Nasreddine Nabi kupindua meza kibabe huko huko Nigeria kwa mujibu wa maoni mbalimbali ya wadau.

Yanga ambao waliondoka juzi usiku nchini kwa ndege ya moja kwa moja ambayo itawasubiri na kurejea nayo mara baada ya mchezo Jumapili, wanakabiliwa na kibarua cha kuibuka na ushindi wa tofauti ya mabao mawili au 2-1, 3-2 ili kutinga raundi ya pili kama watapata bao moja na mchezo kumalizika hivyo itabidi kuongezwa dakika 30 ili kutafutwa mshindi wa jumla.

Aliyekuwa kocha wa zamani wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema fikra na mawazo ya wachezaji wa Yanga wanatakiwa kuona kuwa inawezekana maana kwenye mpira hakuna jambo ambalo linashindana kama ambavyo wapinzani wao walipata bao wakiwa ugenini na kwao inawezekana.

“Ningepata nafasi ya kuongea na wachezaji ningewaeleza kuwa inawezekana kuvuka hatua hii. Tungesema kuwa Yanga wanamlima mrefu wa kupanda kama wangekuwa wamefungwa mabao matatu au manne wakiwa nyumbani lakini moja sio tatizo sana,” alisema.

Mholanzi huyo ambaye makazi yake ni Ghana, aliongeza kwa kusema, “ni vile nipo kwenye maandalizi ya kumpeleka binti yangu Ulaya kusoma lakini nilitamani kuutazama mchezo huo.”

Kwa upande wa kocha msaidizi wa Simba Queens, Matty Msetti Maarufu kama Mattydiola alisema Yanga wanapaswa kuona kuwa huu ndio mchezo wao wa kwanza hivyo wanatakiwa kuwa na mwanzo mzuri hilo litawasaidia kuwa na utulivu pamoja na njaa ya kuanza kwa ushindi.

Advertisement

“Wakipaniki tu watajikuta wakipoteza tena, ni vizuri timu kuandaliwa kisaikolojia na uzuri ni kwamba kikosi chao kinawachezaji wenye uzoefu. Naamini kuwa Yanga inaweza kufanya vizuri hata kama wanacheza ugenini, kikubwa ni kuwa na nidhamu,” alisema kocha huyo.

Kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina, Mohammed Badru ameonyesha kuwa na imani kubwa na Nabi kwa kusema anaweza kuwashangaza wengi kwa kuiongoza Yanga kufanya vizuri wakiwa ugenini, “Nadhani jambo muhimu ni viongozi kumwacha afanye kazi yake, wakianza kumpa presha itaondoa utulivu kwake. Yanga bado nafasi wanayo.”

Author:

Leave a Reply

Your email address will not be published.